Jumapili 26 Aprili 2026 - 21:05
Mustakabali utashuhudia mwisho wa nguvu kubwa za dunia

Hawza/ Hujjat al-Islam wal-Muslimin Sayyid Sadr al-Din al-Qubanchi alisema: Mgongano kati ya uongozi wa kidini na uongozi wa kisiasa umeongezeka, na hili linaashiria mgogoro unaokaribia kupelekea kuporomoka kwa ulimwengu wa Magharibi; mustakabali wa Magharibi utashuhudia mwisho wa nguvu kubwa za dunia.

Kwa mujibu wa ripoti ya kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Hujjat al-Islam wal-Muslimin Sayyid Sadr al-Din al-Qubanchi, Imamu wa Swala ya Ijumaa wa Najaf Ashraf, katika khutba za Swala ya Ijumaa alizozitoa katika Husseiniyya Kuu ya Fatimiyya Najaf Ashraf, alisema: Katika ulimwengu wa Magharibi, yaani Marekani na Ulaya, mgongano kati ya uongozi wa kidini na uongozi wa kisiasa umeongezeka; Papa Leon wa Kumi na Nne bado yuko katika safari ya kihistoria kuelekea bara la Afrika na anakosoa sera za Marekani, pale aliposema: “Dunia inaangamia mikononi mwa kundi la madikteta wanaotumia mamia ya mabilioni ya dola kwa ajili ya vita.” Wakati huo huo, maaskofu wa Marekani wametangaza kumuunga mkono kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, huku Rais wa Marekani akiyakosoa waziwazi matamshi ya Papa.

Aliongeza: Papa hivi karibuni huko Kameroon alisema: “Laana iwe juu ya wale wanaotumia vibaya dini na jina la Mwenyezi Mungu ili kufanikisha malengo yao ya kijeshi, kisiasa na kiuchumi”; “Wao wanafumba macho yao dhidi ya ukweli huu kwamba mabilioni ya dola yanatumika kwa ajili ya mauaji na uharibifu, ilhali fedha hizo zinapaswa kutumika kwenye sekta za afya na elimu.”

Imamu wa Swala ya Ijumaa wa Najaf Ashraf alisisitiza: Maneno haya yanaashiria mgogoro unaokaribia kupelekea kuporomoka kwa ulimwengu wa Magharibi; mustakabali wa Magharibi utashuhudia mwisho wa nguvu kubwa za dunia.

Katika kumbukumbu ya mwaka wa kuuawa kishahidi Shahidi Sadr wa pili, alisema; tunakumbuka jinai za utawala wa Baath

Hujjat al-Islam wal-Muslimin Sayyid Sadr al-Din al-Qubanchi katika sehemu nyingine ya khutba alisema: Katika kumbukumbu ya mwaka wa kuuawa kishahidi kwa Shahidi Sadr wa pili, tunakumbuka jinai za utawala wa Baath. Hapa nasoma barua iliyotolewa na kamanda wa kikosi cha Dhi Qar, iliyowaelekezwa kwa wanamgambo wa kujitolea wa Saddam kwa anuani ya “ta’mim”. Katika barua hiyo imeandikwa: Tarehe 2001/10/3 (mwaka 1379 Hijria Shamsia), hukumu ya kukatwa vidole vya mkono wa kulia wa mhalifu (jina limefutwa) kwa sababu ya kuchana picha ya rais, ilitekelezwa mbele ya mwakilishi msimamizi wa wanamgambo wa Saddam, gavana wa Dhi Qar na katibu wa tawi la chama katika mkoa huo. Barua hii ina tarehe ya 2001/11/1 (1379 Hijria Shamsia) na inahesabiwa kuwa moja ya nyaraka za jinai za utawala wa Saddam aliye laaniwa.

Aligusia pia masuala ya ndani kwa kuashiria kupanda kwa bei na kusema: Hapa kama alivyosema Amir al-Mu’minin (as) katika barua yake kwa Malik al-Ashtar:

“Basi pokea wasia wangu kuhusu wafanyabiashara na wenye fani mbalimbali…” hadi aliposema: “Zuia uhifadhi wa bidhaa (ihtikār), kwa sababu Mtume wa Mwenyezi Mungu (saww) aliukataza, na iwe biashara ni ya urahisi kwa mizani ya uadilifu na bei ambazo hazimuumizi muuzaji wala mnunuzi.” Kisha Imamu (as) akaongeza: “Yeyote atakayefanya ihtikār baada ya wewe kumkataza, basi mshughulikie kwa ukali, lakini bila kupita kiasi.”

Hujjat al-Islam wal-Muslimin Sayyid Sadr al-Din al-Qubanchi aliendelea kusema: Mafaqihi wanasisitiza kuwa, kuuza kwa bei za kupindukia, ambazo zinadhuru soko na mnunuzi, kuna tatizo la kisheria. Kwa sababu hiyo tunaviomba vyombo vya usalama kuwafuatilia wauzaji wanaouza bidhaa kwa bei mara mbili.

Wananchi hawaridhishwi na mzozo huu wa kisiasa kuhusu kucheleweshwa kwa uteuzi wa waziri mkuu

Kuhusu uteuzi wa waziri mkuu, alisema: Wananchi hawaridhishwi na mzozo huu wa kisiasa kuhusu kucheleweshwa kwa uteuzi wa waziri mkuu. Msiruhusu matakwa ya wageni yaondoe uhuru wenu wa kisiasa. Iran kupitia mjumbe wake imetangaza kuwa haiingilii masuala ya ndani na kwamba uamuzi uko mikononi mwa wananchi wenyewe, ilhali Marekani imetuma ujumbe rasmi na kukataa chaguo fulani, na wiki moja baadaye ikatuma ujumbe mwingine wa kukataa mtu mwingine; hili lina maana ya uingiliaji wa moja kwa moja katika mambo ya ndani ya Iraq na ni aina ya shinikizo la kutaka kuathiri matakwa ya waziri mkuu mteule, jambo ambalo tunalikataa kwa msimamo mkali.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha